“DAKIKA 180 GOLGOTHA”
Amithay Hezekiah Kuhanda (PhD)
UTANGULIZI
Maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka 2026 yananifanya kutafakari upya tukio la ukombozi wa mateka (waliotekwa) lijulikanavyo kama ‘Dakika 90 Entebbe’. Tukio hili la kweli la uokoaji wa mateka 103 wa kiyahudi lilitokea tarehe 4 July 1976. Anasimulia Stevenson (1976)[1] kuwa makomandoo wa Israeli walisafiri umbali wa kilomita 4000 kuja kuwakomboa ndugu zao waliokuwa wanashikiliwa na magaidi saba (7) katika uwanja wa ndege Entebbe. Mateka hao walichambuliwa na kushikiliwa kutoka kwenye ndege kubwa ya abiria (Air France, Flight 139) iliyotekwa ikiwa Ugiriki na kuelekezwa Libya, na baadaye Entebbe nchini Uganda.
Makoandoo 100 wa Israeli, walioendesha ‘operesheni thunderbolt’, walifanikiwa kuwaua magaidi wote saba, askari kadhaa wa jeshi la Uganda, na kuwakomboa mateka wote, isipokuwa mateka mmoja aliyekuwa amepelekwa hospitali kutibiwa. Tukio la ‘operation thunderbolt’ lilichukua muda mfupi, dakika 90. Hata hivyo, kiongozi wa operesheni hii, Lt. Col. Jonatan Netanyahu (kaka yake Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israeli) alipigwa risasi na kuuwawa katika dakika za mwisho za operation. Makomandoo wengine 99, na mateka huru 102 walirudi nyumbani kwao salama. Jonatan Netanyahu, kijana mbichi kabisa (alikuwa na umri wa miaka 30) atakumbukwa daima kati ya watu mashujaa walio tayari kumwaga damu yao kulitumikia taifa lao. Kama Jonatan angefufuka leo, dunia nzima ingezizima na kuziimba sifa zake tena.
Kama ilivyo ‘Dakika 90 Entebbe’, sikukuu ya pasaka nayo inafunua tukio la kweli la ‘Dakika 180 Golgota’ (Mat 27:45)[2]. Hii ni simulizi tukio la ukombozi wa mateka wa kiroho tunayoweza kuiita ‘operation Golgotha’ iliyoongozwa na komandoo pekee, Yesu Kristo, mwana wa Daudi. Operesheni Golgotha ilifanyika Israeli miaka zaidi ya 2000 iliyopita ikiwalenga wanadamu wote waliowahi kuzaliwa, wanaozaliwa, na watakaozaliwa siku zijazo.
Tofauti na kile alichokifanya komandoo Jonatan pale Entebbe, Yesu Kristo aliongoza mapambano akiwa peke yake (Mat 26:56b)[3] na (Isa 59:15,16)[4], akafanikiwa kubeba hati ya ukombozi wa maelfu ya watu kutoka kila taifa, kila jamaa na kila lugha duniani (Ufu 5:9,10)[5].
Na kama ilivyotokea kwa komandoo Jonatan, kiongozi wa operation Golgotha alijitoa kufa kwa hiari yake (Yoh 10:14-15,17)[6]. Lakini tofauti kabisa na kifo cha Jonatan, Yesu Kristo alifufuka baada ya kukaa kaburini kwa muda wa siku tatu, na sasa yuko hai mbinguni milele (Ufu 1:17,18)[7].
Kutokana na kazi ya dakika 180 (operation Golgotha); mbingu, dunia, bahari na kuzimu kote kunazizima sifa za Yesu Kristo (Ufu 5:11-14)[8]. Vile vile, matokeo ya operation Golgotha yanaendelea kudhihirika hata leo. Watu wanaomkimbilia wanafunguliwa na kuwekwa huru (Mdo 4:9,10).[9] Kwa sababu hiyo, mtume Paulo anautetea msalaba ifuatavyo:
“Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu” (1 Kor 1:18).
Tafsiri nyingine ya kifungu ‘neno la msalaba’ ni ‘ujumbe wa msalaba’ au ‘kinachobebwa na msalaba’ au ‘siri iliyoko kwenye kazi ya msalaba’. Paulo anataka tujue kuwa ndani ya msalaba kuna ujumbe au taarifa ya thamani kwetu tunaookolewa, ijapokuwa watu wanaopotea (wasiojua bado thamani hiyo) wanaupuuza. Thamani ya kitu chochote hupimwa kwa gharama iliyotumika kukinunua kitu hicho.
Kama gharama ya kukipata kitu ni ndogo basi na thamani ya kitu hicho ni ndogo; na kama gharama yake ni kubwa basi thamani yake ni kubwa. Ujumbe wa Msalaba una thamani kuu, uligharimu maisha ya Yesu Kristo, na nguvu ya kumfufua kutoka kwa wafu. Yafuatayo mambo makuu yatokanayo na kazi ya msalaba (operation Golgotha):
1. NGUVU YA UPATANISHO (KATI YA MUNGU NA MWANADAMU)
Dhambi ilipoingia duniani, ilimtenga mwanadamu na Mungu (pamoja na vyote alivyokuwa navyo). Uwepo wa Mungu uliondoka, kwa mwanadamu na kwa vitu vyote alivyokuwa navyo (Rum 8:19-22). Kwa kazi ya msalaba, Yesu alivipatanisha vitu vyote na nafsi yake, ikiwa ni pamoja na mwanadamu (Kol 1:19-22)[10]. Kwa njia ya msalaba tunarejeshewa utakatifu wa kimungu na tunapatanishwa naye. Mahusiano ya karibu yanarejea tena baina yetu na Mungu.
Katika Agano la Kale (kabla ya msalaba), ilikuwa haiwezekani kwenda mbele za Mungu moja kwa moja, mpaka upitie kwa Kuhani Mkuu; na huyo kuhani mkuu ilikuwa ni lazima atoe sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya dhambi zake na dhambi za wale anaowaongoza ndipo aende mbele za Mungu, na tena huingia mara moja kwa mwaka (Ebr 9:6-9)[11]. Baada ya kazi ya msalaba, kila mmoja ameruhusiwa kwenda mbele za Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Damu ya Yesu inatupa ujasiri na kibali cha kukaribia patakatifu pa patakatifu (Ebr 9:11-14)[12].
Katika Agano Jipya (baada ya kazi ya msalaba), kila mmoja ameruhusiwa kwenda mbele za Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Kupitia kazi ya msalaba, pazia la hekalu (Kut 26:31–35) lilipasuka ndani ya kipindi cha dakika 180 msalabani (Mat 27:51). Hii ilikuwa ni ishara kuwa sasa kila mtu anaruhusiwa kwenda mbele za Mungu bila kuwa na kipingamizi chochote, kupitia damu ya Yesu Kristo. Damu ya Yesu inatupa ujasiri na kibali cha kukaribia patakatifu pa patakatifu [(Warumi 5: 11)[13], (Waebrania 10:19-22)[14]].
Upekee Yesu huduma ya Yesu (akilinganishwa na manabii wengine waliomtangulia, na wanaomfuata) ni pamoja na kuanzisha na kutuachia huduma hiyo ya upatanisho (1 Kor 5:18-19).[15]
2. NGUVU YA UZIMA (DHIDI YA ROHO YA MAUTI)
Mauti ni roho inayohusika kuleta kifo na uharibifu katika maisha ya mwanadamu. Kuna aina mbili za vifo: kifo cha kiroho – ambacho hutenganisha nafsi ya mtu na Mungu wake; na kifo cha kimwili – ambacho hutenganisha nafsi ya mtu na mwili wake.
Nguvu ya mauti ni dhambi. Bwana alionya Adamu kwamba matokea ya kutotii itakuwa kifo (Mwanzo 2:17)[16]. Adamu alipokosa kutii, alipokea kama mshahara kifo cha kiroho mara moja, ambacho kilimfanya ajifiche (Mwanzo 3:8). Baadaye, Adamu alipata mshahara wa kifo cha kimwili (Mwanzo 5:5)[17]. Kupitia Adamu, lango la mauti lilifunguliwa, hivyo mauti ikawapata wanadamu wote. Ulimwengu mzima uko chini ya nguvu ya mauti kwa sababu wote wamefanya dhambi[18].
Kupitia kazi ya msalaba, ilimpasa Yesu (lango la wokovu) kufa (Mat 5:50)[19] kwa niaba ya watu wote, ili kwa kupitia yeye kila mtu apokee nguvu ya uzima[20]. Kupitia msalaba, Yesu aliihukumu roho ya mauti kwa njia ya mauti yake, alitumia mauti kuihukumu mauti. Adamu (na Jonatan) walikufa kwa sababu walikuwa mwenye dhambi, bali Yesu, ambaye hakuwahi kufanya dhambi, alifanywa kuwa dhambi na hivyo kufa kwa niaba ya wenye dhambi.
Ushindi dhidi ya amauti ni kuwa, Yesu alionyesha uwezo wake juu ya mauti kwa kufufuka kutoka kwa wafu (1 Kor 15:20, 22)[21]. Kwa sababu ya kufufuka kwake, na tumaini la ufufuo kwetu kwa sababu yake aliye limbuko lao waliolala, MAUTI NI ADUI ALIYESHINDWA. Kwa wale ambao hawajampokea Yesu Kristo, kifo cha kimwili kinaondoa fursa ya kupokea neema hii ya ukombozi (Ebr 9:27)[22]. Kwa wale waliookoka, kifo cha kimwili kinaleta fursa ya kuwepo pamoja na Bwana (2 Kor 5:8-9)[23], (Fil 1:21-24)[24].
Ahadi ya ufufuo wa kwanza kwa wafu waliookoka ni thabiti kiasi kwamba kifo cha kimwili huitwa "kulala" (1 Kor 15:51)[25]; (Yoh 11:11)[26]. Hata hivyo, tunautazamia wakati ambapo hakutakuwa na mauti iletayo kifo tena (Ufu 21:4)[27].
3. NGUVU YA KUZALIWA UPYA (DHIDI YA UTU WA KALE)
Kazi nyingine ya msalaba ni kushughulikia mabadiliko ya mtu wa ndani ili maisha ya kimwili yabadilike. Hali yetu ya kimwili inategemea sana hali yetu ya kiroho. Kama mtu wa ndani (wewe halisi) hujabadilika na unasema umeokoka, basi kiuhalisia bado hujaokoka. Kuokoka ni kubadilika kwa mtazamo wako na mwenendo wako. Utu wako wa ndani unafanywa upya (Rum 6:1-7)[28].
Yesu alituzaa kwa upya pale msalabani (1 Pet 1:3)[29] na pale msalabani ndiko tulikopata tabia njema, mawazo mema, na mwenendo mpya. Yesu Kristo anapotusamehe dhambi zetu hatuachi tu tukajiongoza wenyewe bali pia nashugulika na kubadilisha utu wetu wa ndani ili tusiwe tena watumwa wa dhambi bali tumtumikie yeye peke yake.
Mabadiliko ya mtu wa ndani sio jitihada zako, bali ni kazi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani (Efe 4:21-24)[30]. Ile kwamba unakataa/unachukia dhambi sio kwamba ni ujanja wako bali ni kazi ya msalaba. Kwa hiyo usijisifu, bali mtukuze Mungu.
4. NGUVU YA UKOMBOZI (DHIDI YA VIFUNGO VYA LAANA)
Laana ni tamko, apizo, hukumu, au hali ya kukosa kibali cha Mungu au watu inayoleta madhara, maangamizi, au vizuizi katika maisha ya mtu, familia, au taifa. Vile vile laana inaweza kutokana na maneno ya watu wenye mamlaka (kama wazazi, wazee wa ukoo, wachawi) yaliyotamkwa kwa uchungu ili mtu afikiwe na mabaya fulani badala ya mema yaliyokusudiwa. Athari za laana hujumuisha magonjwa, kutokufanikiwa, vifo vya mapema, au kuvunjika kwa mahusiano.
Kuna aina kuu nne za vifungo vya laana:
· Kifungo cha laana ya dhambi (Mwanzo 3:16-19)[31]
· Kifungo cha laana ya Torati – torati ni chanzo cha laana kwa yule anayesishi kwa hiyo lakini asiitekeleze kilamilifu (Kol 2:13-17)[32]; (Gal 3:10)[33]
· Kifungo cha laana ya kutokumtegemea Mungu (Yer 17:5)[34]
· Kifungo cha laana za kichawi au ukoo – wachawi au wazee wa ukoo nao pia huweza kusema jambo likatokea kama mtu haishi katika haki na Baraka za Mungu (Hes 22:6)[35]
Mbali na kifo, kuna kiwango cha ustawi katika maisha mwanadanu hawezi kufikia kwa sababu ya laana. Atakifikia tu kama atampokea Yesu (aliyelaaniwa kwa niaba yake) kuwa Bwana na Mwokozi katika maisha yake.
Yesu alipokufa pale msalabani alitutoa kwenye vifungo vya laana mbalimbali zilizokuwa juu ya maisha yetu (Rum 8:33-34)[36]. Kwa lugha nyingine, ndani ya msalaba wa Yesu tunapata mafanikio yetu, tunapata afya, tunapata kustawi, tunapata kuongezeka na kusonga mbele. Lakini lazima tuujue ukweli huu (kwa kukaa ndani ya Yesu) ili tuwekwe huru.
5. NGUVU YA MAMLAKA YA UTAWALA KUREJESHWA
Mwanadamu aliumbwa ili awe nafasi ya mtawala, na alipewa rasmi nguvu na mamlaka ya utawala siku aliyoumbwa (Mwa 1:26)[37]. Hata hivyo, dhambi ilimwondolea nguvu na mamlaka hayo n ahivyo akapoteza nafasi yake (Mwa 3:8-10)[38].
Kupitia Adamu (kwa sababu yeye ni lango), mwanadanu alipoteza nafasi ya kuwa mtawala katika ulimwengu huu. Kupitia kazi ya msalaba, Yesu Kristo alifanyika lango la kumrejeshea mwanadamu aliyeokoka nafasi yake ya utawala katika ulimwengu huu (Ufu 5:10-11)[39]. Kwa maana nyingine, mara tu baada ya kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi, moja ya mambo yanayofanyika juu ya mwamini katika ulimwengu wa roho ni kurejeshea nafasi aliyokuwa umeipoteza hapo mwanzo ulipomuasi Mungu (kupitia Adam kama lango). Shetani anachokifanya leo (kama alivyofanya mwanzo) ni kukupiga vita ili akuondoe kwenye nafasi uliyonayo (wokovu) kwa sababu anajua akikuondolea nafasi uliyonayo popote pale basi hata mamlaka pia itaondoka.
Vile vile, mwenye ufunguo ndiye mwenye mamlaka (Mat 16:18-19)[40], lakini huwezi ukawa na mamlaka kama huna nafasi (cheo), sharti upewe kwanza nafasi (kuwa mwana) ndipo apate uwezo wa kutumia mamlaka yako.
6. NGUVU YA UJASIRI (DHIDI YA HOFU, HUZUNI NA MASIKITIKO)
Nabii Isaya anaandika: Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa (Isaya 53 :4). Kuna vitu vinne ambavyo ni vyanzo vya hofu, huzuni na masikitiko katika maisha ya wanadamu. Msalaba umefanyika kuwa jawabu kama maandiko yanavyosema:
a. a. Mahitaji - Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Rum 8:31,32
b. Dhiki - Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Rum 8:35-37
. c. Hukumu ya adhabu (dhambi zilizotubiwa) - Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Rum 8:33,34
d. Hukumu ya adhabu (kutotimiza matakwa ya totati) - Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo. Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. Kol 2:13-17
7. NGUVU YA JINA LA YESU (ZAO LA UNYENYEKEVU KATIKA MSALABA)
Thamani na nguvu ya Jina la Yesu inatokana na unyenyekevu na utii wa Yesu kupitia njia ya msalaba/ Alikubali kufa mauti ya msalaba.
Maombi ya Gethsemane
- Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Mat 26:39.
- Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. Mat 26:41.
- Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. Mat 26:41
Unyenyekevu
“…bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. (Fil 2:7-8).
Jina lenye Nguvu – kama matokeo ya unyenekevu
Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” (Fil 2:9-11).
Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo. Isa 9:6-7.
Tumepewa Jina hilo!
Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu WALILOPEWA WANADAMU litupasalo sisi kuokolewa kwalo. (Matendo 4:12)
Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. Mk 16:17-18.
Msalaba unamtofautisha Yesu na manabii wengine
Kama Yesu asingekufa msalabani, tungemfananisha na manabii wengine. Msalaba ndio unaomtambulisha na kumtofautisha na manabii wengine waliomtangulia, na waliomfuata baadaye (Mat 16:13-16)[41]. Wako manabii waliotenda miujiza ambayo ilikaribiana na aliyoitenda Yesu, wapo waliofufua wafu, wapo walioponya watu, wapo waliofanya ishara kubwa na za ajabu zinazokaribiana na alizofanya Yesu. Tofauti ya Yesu na hao manabii ipo kwenye kazi ya msalaba.
HITIMISHO
Lt. Col. Jonatan Netanyahu aliongoza ukombozi kimwili kwa ndugu zake 102 kwa gharama ya kifo, akisaidiwa na askari wenzake 99. Kama mwanadamu mwenzetu, hakufufuka. Kwa upande mwingine, Yesu Kristo mwana wa Mungu, akiwa pekee, alileta na anaendelea kuleta ukombozi wa kimwili na kiroho kwa watu wasiohesabika (Ufu 7:9,10)[42] kwa gharama ya kifo cha aibu. Yesu Kristo alifufuka siku ya tatu, yupo hai leo, na anastahili kupokea sifa zote!
Kwetu sisi, baada ya kutendewa haya yote na mwokozi Yesu Kristo, mwitikio wetu ni upi? Mzaburi anatushauri cha kufanya anaposema: Nimrudishie Bwana nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; Na kulitangaza jina la Bwana (Zab 116:12-13). Kuupokea wokovu (kuokoka), na kuanza kutangaza sifa zake (ambazo ndizo ujumbe wa msalaba) ni mwitikio ambao Bwana Yesu anautarajia kutoka kwetu. Amina.
KUHUSU MWANDISHI
Dr Amithay ni mkufunzi na Mkuu wa Chuo cha Biblia cha Hezekiah Kuhanda Bible School Foundation. Kwa mawasiliano zaidi tumia njia zifuatazo:
Tovuti: www.hkbsf.ac.tz
Email: info@hkbsf.ac.tz
Simu: 0756 792 562
Kuna madirisha mawili ya kusajiri wanafunzi kila mwaka: mwezi Februari na mwezi Mei.
Karibu tujifunze maneno ya Mungu pamoja.
BIBLIA MWANGA WAKO!!
[1] https://www.amazon.com/90-Minutes-Entebbe-Spectacular-Counterterrorism/dp/1629144428
[2] Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Mathayo 27:45.
[3] Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Mathayo 26:56b.
[4] Akaona ya kuwa hapana mtu, akastaajabu kwa kuwa hapana mwombezi; basi, mkono wake mwenyewe ndio uliomletea wokovu; na haki yake ndiyo iliyomsaidia. Akajivika haki kama deraya kifuani, na chapeo cha wokovu kichwani pake, akajivika mavazi ya kisasi yawe mavazi yake, naye alivikwa wivu kama joho. Isaya 59:15,16
[5] Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi. Ufunuo 5:9,10
[6] Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Yohana 10:14-15,17.
[7] Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. Ufunuo 1:17,18.
[8] Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka. Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele. Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu. Ufunuo 5:11-14.
[9] kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Matendo 4:9,10
[10] Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni. Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama; (Kol 1:19-22).
[11] Basi, vitu hivi vikiisha kutengenezwa hivyo, makuhani huingia katika hema hiyo ya kwanza daima, wakiyatimiza mambo ya ibada. Lakini katika hema hiyo ya pili kuhani mkuu huingia peke yake, mara moja kila mwaka; wala si pasipo damu, atoayo kwa ajili ya nafsi yake na kwa dhambi za kutokujua za hao watu. Roho Mtakatifu akionyesha neno hili, ya kwamba njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa haijadhihirishwa bado, hapo hema ya kwanza ilipokuwa ingali ikisimama; ambayo ndiyo mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa, zisizoweza kwa jinsi ya dhambi kumkamilisha mtu aabuduye, (Ebr 9:6-9)
[12] Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai? (Ebr 9:11-14)
[13] Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho. (Rum 5:11)
[14] Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi. (Ebr 10:19-22).
[15] Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. 1 Kor 5:18-19
[16] Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. (Mwanzo 2:17)
[17] Siku zote za Adamu alizoishi ni miaka mia kenda na thelathini, naye akafa. Mwanzo 5:5.
[18] Kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na kwa njia hiyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi. Warumi 5:12.
[19] Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Mat 27:50.
[20] ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Ebr 2:9
[21] Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. 1 Kor 15:20, 22.
[22] Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; 28 kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu. Ebr 9:27.
[23] Lakini tuna moyo mkuu; nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana. Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye. 2 Kor 5:8,9
[24] Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu. Fil 1:21-24
[25] Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika. 1 Kor 15:51
[26] Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. Yoh 11:11
[27] Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Ufu 21:4
[28] Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi. (Rumi 6:1-7)
[29] Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; 1 Pet 1:3.
[30] …mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. Efe 4:22-24
[31] Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi. Mwa 3:16-19.
[32] Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo. Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. Kol 2:13-17
[33] Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Gal 3:10.
[34] Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Yer 17:5,6.
[35] Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa. Hes 22:6
[36] Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Rum 8:33-34
[37] Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mwa 1:26.
[38] Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone. Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Mwa 3:8-10.
[39] Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi. (Ufu 5:10-11).
[40] Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. (Mat 16:18-19).
[41] Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. (Mat 16:13-16)
[42] Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo. (Ufu 7:9,10).

Comments
Post a Comment