“DAKIKA 180 GOLGOTHA” Amithay Hezekiah Kuhanda (PhD) UTANGULIZI Maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka 2026 yananifanya kutafakari upya tukio la ukombozi wa mateka (waliotekwa) lijulikanavyo kama ‘Dakika 90 Entebbe’. Tukio hili la kweli la uokoaji wa mateka 103 wa kiyahudi lilitokea tarehe 4 July 1976. Anasimulia Stevenson (1976) [1] kuwa makomandoo wa Israeli walisafiri umbali wa kilomita 4000 kuja kuwakomboa ndugu zao waliokuwa wanashikiliwa na magaidi saba (7) katika uwanja wa ndege Entebbe. Mateka hao walichambuliwa na kushikiliwa kutoka kwenye ndege kubwa ya abiria (Air France, Flight 139) iliyotekwa ikiwa Ugiriki na kuelekezwa Libya, na baadaye Entebbe nchini Uganda. Makoandoo 100 wa Israeli, walioendesha ‘operesheni thunderbolt’, walifanikiwa kuwaua magaidi wote saba, askari kadhaa wa jeshi la Uganda, na kuwakomboa mateka wote, isipokuwa mateka mmoja aliyekuwa amepelekwa hospitali kutibiwa. Tukio la ‘operation thunderbolt’ lilichukua muda mfupi, dakika 90. ...